THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

MINISTRY OF NATURAL RESOURCES AND TOURISM

WANANCHI WA KIJIJI CHA SHIGELA- BUSEGA WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA FISI

October 6, 2025

Share To

Wananchi wa Kijiji cha Shigela Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya fisi wanaovamia makazi ya watu.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Bw. Lusato Masinde katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Shigela leo Oktoba 6, 2025 ambapo timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, TAWA na Maafisa Wanyamapori wa Halmashauri inaendelea kutoa elimu ya uhifadhi Mkoani Simiyu.

“Tuchukue tahadhari kubwa hatuko salama kwa sababu katika mazingira yetu hawa wanyamapori wapo na kuna vichaka na mapango mengi” amesisitiza Bw. Masinde.

Aidha, amewataka wananchi kuongeza jitihada katika kuwalinda watoto dhidi ya fisi hao kwa kuwa wao ni waathirika wakubwa.

Naye, Afisa Maliasili kutoka Wilaya ya Busega, Bi. Jesca Mathias amesema kuwa kutokana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu Mkoani Simiyu, Serikali inalipa kifuta jasho/machozi kwa waathirika.

Amewataka wananchi hao kuhakikisha wanatoa taarifa za majeruhi, vifo au uharibifu wa aina yoyote unaotokana na wanyamapori wakali na waharibifu ili taratibu za malipo zifanyike kwa wakati.

“Unapotoa taarifa mapema kwa kiongozi wa kijiji zitajazwa fomu maalum za malipo ambazo zitapelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii ” amesema Bi. Jesca.

Kwa upande wake Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Nassoro Wawa amesema Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kukusanya taarifa za wananchi wanaopata athari kutokana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu. Ni mfumo ambao taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu zitatumwa moja kwa moja kutoka uwandani na maafisa wanyamapori, kilimo na mifugo utarahisisha malipo ya kifuta jasho na machozi.

Elimu ya uhifadhi na namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu inaendelea kutolewa Mkoani Simiyu lengo ikiwa ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuepuka madhara yatokanayo na wanyamapori hao.

Share To