Wananchi wa vijiji vya Nyantugutu, Lung’wa na Nding’ho vya
Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu wameipongeza Serikali kwa kuunda na kuboresha
mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za wanyamapori wakali na waharibifu (Problem
animal information system- PAIS) ambao umerahisisha malipo ya kifuta
jasho/machozi pindi madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu yanapotokea kwa
wananchi.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ndi’hgo , Bi.
Salome Kambona katika mkutano wa hadhara wa kuelimisha wananchi namna ya
kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu uliofanyika
kijiji cha Ndi’hgo ,Wilaya ya Itilima leo Oktoba 9, 2025.
“Tunaishukuru Serikali kwa mfumo huu ambao ndani ya
siku saba mwananchi atatakiwa awe ametoa taarifa ya madhara yaliyotokana na
mnyamapori ili aweze kulipwa” amesema Bi.Salome.
Naye, Mkazi wa Kijiji cha Nyantugutu, Bw. Mosses Saguda
amesema mfumo wa PAIS umepunguza urasimu na usumbufu wa malipo.
“Tunaishukuru Serikali kwa utaratibu mpya wa mfumo wa
malipo ya kifuta jasho/machozi kwani hauna usumbufu wowote na tunalipwa kwa
simu au benki tofauti na awali tulikuwa tunakaa mwaka bila kulipwa”
amesema Bw. Saguda.
Aidha, ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuweka utaratibu
wa malipo ya kifuta jasho kwa wananchi wanaoharibiwa mazao yakiwa ghalani.
Akizungumza kuhusu elimu hiyo kwa wananchi, Afisa
Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Nassoro Wawa amesema
matarajio ya Serikali baada ya mafunzo hayo ni wananchi kupata uelewa wa
kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kujua sheria, kanuni
na taratibu za namna ya kumiliki wanyamapori kwa sababu mnyamapori ni nyara za
Serikali.
“Pia tumewaeleza fursa zinazopatikana hususan kuanzisha
bucha za wanyamapori, bustani na ranchi za wanyamapori ili waweze kujipatia
vipato” amesisitiza Bw. Wawa.
Elimu hiyo unatolewa Mkoani humo kufuatia matukio ya
wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo,fisi, mamba na viboko.