Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi leo Oktoba 8, 2025 ameshiriki uzinduzi wa programu tumizi (App) iitwayo “Tanapa Go”iliyo chini ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Abbasi amewapongeza TANAPA kwa ubunifu huo na kuzitaka taasisi nyingine za utalii kwenda kidigitali maana takwimu zinaonesha karibu robo tatu ya dunia iko mtandaoni.
“Nawapongeza TANAPA kwa ubunifu huu mkubwa utakaosaidia kutangaza zaidi vivutio vyake na hivyo kuvifanya kuwa mashuhuri barani Afrika na duniani kiujumla na kuweza kutembelewa na idadi kubwa ya wageni,” amesema Dkt. Abbasi.
Programu Tumizi hiyo ya ‘TANAPA Go’ itamwezesha mtalii kupata huduma na taarifa zote muhimu kuhusu hifadhi zetu kwa urahisi mkubwa ikiwemo kupata taarifa za vivutio vyote vya Hifadhi za Taifa 21 na maeneo 5 ya Malikale ambayo TANAPA imekasimiwa kusimamia.
Hafla hiyo iliyofanyika katika Hifadhi ya Mikumi imehudhuriwa na wadau mbalimbali wa utalii na uhifadhi.