THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

MINISTRY OF NATURAL RESOURCES AND TOURISM

Na Saidi Lufune, Dodoma

WIZARA ya Maliasili na Utalii imepokea timu ya ukaguzi kutoka Tume ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa kawaida kuhusu uzingatiaji wa sheria na taratibu za usimamizi wa utumishi wa umma kwa mwaka wa fedha 2025/2026, unaoanza Julai hadi Desemba 2025.

Akizungumza wakati wa kikao cha ufunguzi wa zoezi hilo leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo, Abdallah Mvungi, amesema wizara imedhamiria kushirikiana kikamilifu na timu ya ukaguzi ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi na kwa uwazi.

Mvungi amebainisha kuwa ukaguzi huo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha uwajibikaji, uadilifu na utawala bora vinaendelea kudumishwa katika wizara hiyo.

“Timu hii imekuja kusaidia kubaini maeneo yanayohitaji maboresho. Ni jukumu letu kuwapa taarifa sahihi na kwa wakati ili kufanikisha kazi yao,” amesema Mvungi.

Aidha, amefafanua zoezi hilo litasaidia kuimarisha mifumo ya kiutawala, kuboresha utoaji huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali watu ndani ya wizara.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Agnes Kapfusi, amesema ukaguzi huo utahusisha maeneo kumi (10) muhimu yanayohusiana na usimamizi wa watumishi wa umma ambayo ni pamoja na
ajira mpya, upandishaji vyeo, likizo za mwaka, nidhamu za watumishi, mafunzo na maendeleo ya watumishi.

Aidha, Kapfusi amesema maeneo mengine ni uzingatiaji wa maadili na usimamizi wa malalamiko, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, masuala ya anuai ya jamii, fidia za ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, pamoja na fao la mwisho wa ajira.

Amesema timu hiyo pia itafuatilia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, ikiwa ni sehemu ya kujiridhisha na utekelezaji wa sheria za ajira na ajira salama kwa watumishi wote wa wizara hiyo.